The chat will start when you send the first message.
1Kristo aliteseka alipokuwa katika mwili wake. Hivyo mjitayarishe kwa fikra ile ile aliyokuwa nayo Kristo. Yeyote anayekubali kuteseka katika maisha haya hakika ameamua kuacha kutenda dhambi.
2Jiimarishe wenyewe ili mweze kuishi maisha yenu yaliyosalia hapa duniani kwa kutenda yale anayotaka Mungu, siyo maovu ambayo watu wanataka kufanya.
3Huko nyuma mmepoteza muda mwingi mkitenda yale ambayo wasiyomjua Mungu wanapenda kutenda. Mliishi kwa kutojali maadili, mkitenda maovu mliyotaka kutenda. Daima mlikuwa mnalewa, mlifanya sherehe mbaya za ulevi, na mlitenda mambo ya aibu katika ibada zenu za sanamu.
4Na sasa “marafiki” zenu wa zamani wanaona ni ajabu kwamba ninyi hamshirikiani nao katika njia za maisha zilizo mbaya na zisizofaa wanazozifuata. Na hivyo wanasema mabaya juu yenu.
5Lakini itawalazimu kukutana na Mungu na kutoa maelezo juu ya yale waliyoyatenda. Yeye ndiye atakaye hukumu watu wote muda si mrefu, walio hai sasa na wale waliokwisha kufa.
6Walikosolewa na wengine katika maisha yao hapa duniani. Lakini ulikuwa mpango wa Mungu kwamba wasikie Habari Njema kabla hawajafa ili wawe na maisha mapya katika Roho.
7Wakati wa kila kitu kufikia mwisho wake umekaribia. Hivyo iweni waangalifu katika akili zenu na mjizuie kwa kila jambo. Hii itawasaidia katika maombi yenu.
8Jambo lililo muhimu kuliko yote, daima mpendane ninyi kwa ninyi kikamilifu, kwa sababu upendo huwawezesha kusamehe dhambi.
9Mkaribishane ninyi kwa ninyi katika nyumba zenu na kushiriki chakula kwa pamoja pasipo manunguniko.
10Mungu amewapa neema yake kwa namna nyingi mbalimbali. Hivyo muwe watumishi wema na kila mmoja wenu atumie kipawa chochote alichopewa kwa njia iliyo bora katika kuhudumiana ninyi kwa ninyi.
11Ikiwa kipawa chako ni kuhubiri, maneno yako yawe kama yanayotoka kwa Mungu. Ikiwa kipawa chako ni kuhudumu, unatakiwa kuhudumu kwa nguvu anazokupa Mungu. Ndipo Mungu atakaposifiwa kwa kila jambo katika Yesu Kristo. Uwezo na utukufu ni wake milele na milele. Amina.
12Rafiki zangu, msishangae kwa sababu ya mateso mnayoyapata sasa, mateso hayo yanaijaribu imani yenu. Msidhani kuwa linalotokea kwenu ni jambo la ajabu.
13Lakini mnapaswa kufurahi kwa kuwa mnayashiriki mateso ya Kristo. Mtafurahi na kujawa na raha wakati uweza wake mkuu utapodhihirishwa kwa ulimwengu.
14Mhesabu kuwa ni heshima watu wanapowanenea mabaya kwa sababu mnamwakilisha Kristo. Linapotokea hilo inaonesha kuwa Roho wa Mungu, aliye Roho wa utukufu, yupo pamoja nanyi.
15Mnaweza kupata mateso; lakini msiteseke kwa sababu mmeua, mmeiba, mmesababisha ghasia, au mmejaribu kutawala maisha ya watu wengine.
16Lakini endapo utateswa kwa kuwa ni “Mkristo” basi usione haya. Bali umshukuru Mungu kwa kuwa unalibeba jina hilo.
17Wakati wa kuanza hukumu umewadia. Hukumu hiyo itaanza na familia ya Mungu. Ikiwa itaanzia kwetu, nini kitawatokea wale wasioikubali Habari Njema ya Mungu?
18“Iwapo ni vigumu hata kwa mtu mwema kuokolewa,
nini kitatokea kwa yule aliye kinyume na Mungu na amejaa dhambi?”
19Hivyo kama mnateseka kwa sababu ya kutii mapenzi ya Mungu, yakabidhini maisha yenu kwake maana Yeye ndiye aliyewaumba, na hivyo mnapaswa kumwamini. Na anastahili kuthaminiwa na kuaminiwa.