1 Wathesalonike 3

1 Wathesalonike 3

1-2Nisingeweza kuja kwenu, ila ilikuwa vigumu kuendelea kusubiri zaidi. Hivyo tuliamua kumtuma Timotheo kwenu na tukabaki Athene peke yetu. Timotheo ni ndugu yetu. Ni mtenda kazi pamoja nasi kwa ajili ya Mungu katika kuwahubiri watu Habari Njema kuhusu Kristo. Nilimtuma Timotheo kuwaimarisha na kuwafariji katika imani yenu.

3Tulimtuma ili asiwepo kati yenu atakayebugudhiwa na mateso tuliyo nayo sasa. Ninyi wenyewe mnatambua kuwa ni lazima tupatwe na mateso haya.

4Hata pale tulipokuwa pamoja nanyi, tuliendelea kuwaeleza mapema ya kuwa sote tutapata matatizo. Na mnafahamu kuwa ilitokea kama tulivyowaambia.

5Hii ndiyo sababu nilimtuma Timotheo kwenu, ili nipate kujua juu ya uaminifu wenu. Nilimtuma kwenu nilipokuwa siwezi kuendelea kusubiri zaidi. Nilihofu kuwa Shetani angeweza kuwashinda kwa majaribu yake. Kisha kazi yetu iliyokuwa ngumu ingepotea bure.

6Bali sasa Timotheo amerudi kutoka kwenu na kutueleza juu ya uaminifu wenu na upendo wenu. Ametueleza kuwa mmeendelea kuwa na kumbukumbu njema juu yetu kama mfano kwenu. Na amesema kuwa mnatamani sana kutuona tena. Hivyo ndivyo ilivyo kwetu pia tunatamani sana kuwaona ninyi.

7Kwa hiyo, ndugu zangu, tunatiwa moyo sana kwa ajili ya uaminifu wenu. Tunapata mateso na masumbufu mengi, lakini bado tunatiwa moyo nanyi.

8Kwa kuwa sasa tuna maisha mapya tunapata utimilifu ikiwa imani yenu katika Bwana inaendelea kuwa imara.

9Tuna furaha tele mbele za Mungu wetu kwa ajili yenu! Lakini hatuwezi kumshukuru Mungu inavyopasa kwa furaha ile yote tuliyo nayo.

10Usiku na mchana tuliendelea kuomba kwa mioyo yetu yote kwamba tuweze kuja huko na tuwaone tena. Tunataka kuwapa kila mnachohitaji ili imani yenu iwe timilifu.

11Tunaomba kwamba Mungu wetu aliye Baba yetu, na Bwana Yesu wataiongoza njia yetu kuja kwenu.

12Tunaomba kuwa Bwana ataufanya upendo wenu uendelee kukua. Tunaomba kuwa atawapa kupendana zaidi na zaidi miongoni mwenu na kwa watu wote. Tunaomba kuwa mtampenda kila mmoja kwa namna ile ile ambayo sisi tuliwapenda ninyi.

13Hii itaongeza hamu yenu ya kutenda yaliyo haki, na mtakuwa watakatifu msio na kosa mbele za Mungu wetu na baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapo kuja na watakatifu wake wote.[#3:13 Au “malaika watakatifu”.]

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International