2 Yohana 1

2 Yohana 1

1Salamu kutoka kwa mzee.[#1:1 Huyu huenda alikuwa ni Mtume Yohana. “Mzee” ina maana ya mtu aliye mtu mzima au kiongozi maalumu katika kanisa (kama vile katika Tit 1:5).]

Kwa mwanamke aliyechaguliwa na Mungu na kwa wanawe.

Kweli kabisa, ninawapenda ninyi nyote. Na sio mimi peke yangu. Bali wote wanaoifahamu kweli wanawapenda vile vile.

2Tunawapenda kwa sababu ya kweli, ile kweli iliyomo ndani yetu. Kweli inayoendelea kuwemo ndani yetu milele yote.

3Neema, rehema, na amani itakuwa pamoja nasi kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa mwanaye, Yesu Kristo, kwa kadri tuishivyo katika kweli na upendo.

4Nilikuwa na furaha sana baada ya kufahamu habari za baadhi ya watoto wako. Nina furaha kuwa wanaifuata njia ya kweli, kama vile baba alivyo tuamuru.

5Na sasa, mwanamke mwema, nina ombi hili: na tupendane sisi kwa sisi. Hii si amri mpya. Ni amri ile ile tuliyo kuwa nayo tangu mwanzo.

6Na hii ndiyo maana ya kupenda: kuishi kulingana na amri zake. Na amri ya Mungu ni hii: Kwamba muishi maisha ya upendo. Mliisikia amri hii toka mwanzo.

7Walimu wengi wa uongo wamo duniani sasa. Wana kataa kusema Yesu ni Masihi aliyekuja duniani na kufanyika mwanadamu. Kila anayekataa kuikubali kweli hii ni mwalimu wa uongo na adui wa Kristo.

8Muwe waangalifu! Msiipoteze thawabu tuliyokwisha kuitendea kazi. Mhakikishe mnaipokea thawabu kamili.[#1:8 Nakala zingine za Kiyunani zina “mliyoyatenda”.]

9Kila mmoja aendelee kuyashika mafundisho aliyefundishwa juu Kristo tu. Yeyote atakayeyabadili mafundisho hayo hana Mungu. Kila anayeendelea kuyafuata mafundisho ya Kristo anao wote Baba na Mwanaye.[#1:9 Hii ilihusu mafundisho juu ya Kristo kama alikuwa mwanadamu na pia Mungu na pia mafundisho ambayo Kristo mwenyewe aliyafundisha.]

10Msiwakubali wale wanaowaijia lakini hawawaletei mafundisho haya. Msiwakaribishe katika nyumba zenu. Msiwape salamu zenu.

11Kama mkiwakaribisha na kuwasalimu, mnawasaidia katika kazi zao za uovu.

12Nina mengi ya kuwaambia. Lakini sitaki kutumia karatasi na wino. Badala yake, nataraji kuja kuwatembelea. Kisha tunaweza kujumuika pamoja na kuzungumza uso kwa uso. Ndipo furaha yetu itakamilika.

13Watoto wa dada yako aliyechaguliwa na Mungu wamekutumia upendo wao.[#1:13 Dada wa mwanamke “mwanamke” katika mstari wa 1. Huyu aweza kuwa mwanamke mwingine au kanisa lingine.]

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International