Matendo 21

Matendo 21

Paulo Aenda Yerusalemu

1Baada ya kuwaaga wazee tulitweka tanga moja kwa moja kwenda kwenye kisiwa cha Kosi. Siku iliyofuata tulikwenda kisiwa cha Rhode na kutoka pale tulikwenda Patara.

2Tulipata meli hapo iliyokuwa inakwenda maeneo ya Foeniki. Tukapanda meli na tukatweka tanga kuondoka.

3Tulitweka tanga na kusafiri karibu na kisiwa cha Kipro. Tuliweza kukiona upande wa kaskazini, lakini hatukusimama. Tulisafiri mpaka katika jimbo la Shamu. Tulisimama Tiro kwa sababu meli ilitakiwa kupakua mizigo yake pale.

4Tuliwapata wafuasi wa Bwana pale na tukakaa pamoja nao kwa siku saba. Walimuonya Paulo asiende Yerusalemu kwa sababu ya kile walichoambiwa na Roho Mtakatifu.

5Lakini muda wetu wa kukaa pale ulipokwisha, tulirudi kwenye meli na kuendelea na safari yetu. Wafuasi wote, hata wanawake na watoto walikuja pamoja nasi pwani. Tulipiga magoti ufukweni sote, tukaomba,

6na tukaagana. Kisha tukaingia melini, na wafuasi wa Bwana wakarudi nyumbani.

7Tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro na kwenda katika mji wa Ptolemai. Tuliwasalimu waamini pale na kukaa nao kwa siku moja.

8Siku iliyofuata tuliondoka Ptolemai na kwenda katika mji wa Kaisaria. Tulikwenda nyumbani kwa Filipo na kukaa kwake, alikuwa mhubiri wa Habari Njema. Alikuwa mmoja wa wasaidizi saba.[#21:8 Wanaume waliochaguliwa kwa ajili ya kufanya kazi maalumu. Tazama Mdo 6:1-6.]

9Alikuwa na mabinti wanne mabikira waliokuwa na karama ya kutabiri.

10Baada ya kuwa pale kwa siku kadhaa, nabii aliyeitwa Agabo alikuja kutoka Uyahudi.

11Alikuja Kwetu na kuazima mkanda wa Paulo. Aliutumia mkanda huo na akajifunga mikono na miguu yake mwenyewe. Kisha akasema, “Roho Mtakatifu ananiambia, ‘Hivi ndivyo ambavyo Wayahudi walioko Yerusalemu watamfunga mtu anayeuvaa mkanda huu. Kisha watamkabidhi kwa watu wasiomjua Mungu.’”[#21:11 Yaani mkanda wa Paulo; Agabo alimaanisha kuwa Wayahudi walioko Yerusalemu watamkamata na kumfunga Paulo.]

12Tuliposikia hili, sisi na wafuasi wengine pale tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu.

13Lakini Paulo alisema, “Kwa nini mnalia na kunihuzunisha? Niko radhi kufungwa Yerusalemu. Niko tayari hata kufa kwa ajili ya jina la Bwana Yesu!”

14Hatukuweza kumshawishi asiende Yerusalemu. Hivyo tuliacha kumsihi na tukasema, “Tunaomba lile alitakalo Bwana lifanyike.”

15Baada ya hili, tulijiandaa na kuelekea Yerusalemu.

16Baadhi ya Wafuasi wa Yesu kutoka Kaisaria walikwenda pamoja nasi. Wafuasi hawa walitupeleka nyumbani kwa Mnasoni, mtu kutoka Kipro, ambaye alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kuwa wafuasi wa Yesu. Walitupeleka nyumbani kwake ili tukae pamoja naye.

Paulo Amtembelea Yakobo

17Ndugu na dada wa Yerusalemu walitukabisha kwa furaha sana walipotuona.

18Siku iliyofuata Paulo alikwenda pamoja nasi kumtembelea Yakobo. Wazee wote walikuwepo pia.

19Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwaambia hatua kwa hatua yote ambayo Mungu aliyatenda katikati ya watu wasio Wayahudi kupitia huduma yake.

20Viongozi waliposikia hili, wakamsifu Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu yetu, unaweza kuona maelfu ya Wayahudi wamekuwa waamini, lakini wanadhani ni muhimu kutii Sheria ya Musa.

21Wameambiwa kuwa unawafundisha Wayahudi wanaoishi katika majimbo yasiyo ya Kiyahudi kuacha kufuata Sheria ya Musa. Wamesikia kuwa unawaambia wasiwatahiri watoto wao na wasifuate desturi zetu.

22Tufanye nini? Wafuasi wayahudi hapa watajua kuwa umekuja.

23Hivyo tutakwambia nini cha kufanya: Watu wanne miongoni mwa watu wetu wameweka nadhiri kwa Mungu.[#21:23 Pengine ni nadhiri ya Mnazareti, wakati maalumu wa kujiweka wakfu na huduma kwa Mungu. Tazama katika Orodha ya Maneno.]

24Wachukue watu hawa walio pamoja nawe na ushiriki katika ibada ya utakaso. Lipia gharama zao ili wanyoe nywele za vichwa vyao. Hili litathibitisha kwa kila mmoja kuwa mambo waliyosikia kuhusu wewe si sahihi. Watajua kuwa wewe mwenyewe unaitii Sheria ya Musa katika maisha yako.[#21:24 Vitu muhimu ambavyo Wayahudi walifanya ili kuikamilisha nadhiri ya mnadhiri. Tazama katika Orodha ya Maneno. Pia katika mstari wa 26.]

25Tumekwisha watumia barua waamini wasio Wayahudi kuwaambia ambayo hawapaswi kufanya:

‘Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu.

Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama zilizo na damu ndani yake.

Wasijihusishe na uzinzi.’”

Paulo Akamatwa

26Hivyo Paulo akawachukua wale watu wanne aliokuwa pamoja nao. Siku iliyofuata alishiriki kwenye ibada ya kuwatakasa. Kisha akaenda eneo la Hekalu na kutangaza siku ya mwisho ambapo kipindi cha utakaso kitakwisha na kwamba sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wa watu hao siku hiyo.

27Siku saba zilipokuwa zinakaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walimwona Paulo katika eneo la Hekalu. Wakamshawishi kila mtu, kisha wakakusanyika kama kundi wakiwa na hasira, kisha wakamkamata Paulo

28na wakapiga kelele wakisema, “Watu wa Israeli, tusaidieni! Huyu ndiye mtu anayefundisha mambo yaliyo kinyume na Sheria ya Musa, kinyume na watu wetu, na kinyume na Hekalu letu. Hivi ndivyo anavyowafundisha watu kila mahali. Na sasa amewaleta baadhi ya Wayunani katika eneo la Hekalu na amepanajisi mahali hapa patakatifu!”

29(Wayahudi walisema hili kwa kuwa walimwona Trofimo akiwa na Paulo Yerusalemu. Trofimo alikuwa mwenyeji wa Efeso, Wayahudi walidhani kuwa Paulo alikuwa amempeleka eneo takatifu la Hekalu.)

30Watu katika mji wote wakajaa hasira, na kila mtu akaja akikimbilia kwenye Hekalu. Wakamkamata Paulo na kumtoa nje ya eneo takatifu, malango ya Hekalu yakafungwa saa hiyo hiyo.

31Walipokuwa wanajaribu kumwua Paulo, Kamanda wa jeshi la Rumi katika mji wa Yerusalemu akapata taarifa kuwa ghasia zilikuwa zimeenea mji wote.

32Mara hiyo hiyo kamanda alikimbilia mahali ambako umati wa watu ulikuwa umekusanyika, aliwachukua baadhi ya maofisa wa jeshi na askari. Watu walipomwona kamanda na askari wake waliacha kumpiga Paulo.

33Kamanda alikwenda mahali alipokuwa Paulo na akamkamata. Akawaambia askari wake wamfunge kwa minyororo miwili. Kisha akauliza, “Mtu huyu ni nani? Amefanya nini kibaya?”

34Baadhi ya watu pale walipiga kelele wakisema kitu hiki na wengine walisema kingine. Kwa sababu ya kuchanganyikiwa huku na kelele kamanda hakujua ukweli kuhusu kilichotokea. Hivyo akawaambia askari wamchukue Paulo mpaka kwenye jengo la jeshi.

35-36Umati wote ulikuwa unawafuata. Askari walipofika kwenye ngazi ilibidi wambebe Paulo. Walifanya hivi ili kumlinda, kwa sababu watu walikuwa tayari kumwumiza. Watu walikuwa wanapiga kelele wakisema, “Auawe!”

37Askari walipokuwa tayari kumwingiza Paulo kwenye jengo la jeshi, Paulo alimwuliza kamanda akasema, “Je! ninaweza kukwambia kitu?”

Kamanda akasema, “Kumbe, unaongea Kiyunani?

38Kwa hiyo wewe si mtu niliyemdhania. Nilidhani wewe ni Mmisri aliyeanzisha vurugu dhidi ya serikali siku si nyingi na akawaongoza magaidi elfu nne kwenda jangwani.”

39Paulo akasema, “Hapana, Mimi ni Myahudi kutoka Tarso katika jimbo la Kilikia. Ni raia wa mji ule muhimu. Tafadhali niruhusu niseme na watu.”

40Kamanda akamwambia Paulo unaweza kusema. Hivyo Paulo akasimama kwenye ngazi na kupunga mkono wake ili watu wanyamaze. Watu walinyamaza na Paulo akaanza kusema nao kwa Kiaramu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International