The chat will start when you send the first message.
1Paulo akasema, “Baba zangu na kaka zangu, nisikilizeni! Nitajitetea kwenu.”
2Wayahudi walipomsikia Paulo anazungumza kwa Kiaramu wakanyamaza. Kisha Paulo akasema,
3“Mimi ni Myahudi, nilizaliwa katika mji wa Tarso katika jimbo la Kilikia. Nilikulia hapa katika mji huu. Nilikuwa mwanafunzi wa Gamalieli ambaye kwa umakini alinifundisha kila kitu kuhusu sheria ya baba zetu. Daima nimekuwa na shauku ya kumheshimu Mungu, sawa na ninyi nyote hapa leo.[#22:3 Alikuwa mwalimu muhimu sana wa Mafarisayo, Kikundi cha kidini cha Wayahudi. Tazama Mdo 5:34.]
4Niliwatesa watu walioifuata Njia. Baadhi yao hapa waliuawa kwa sababu yangu. Niliwakamata wanaume na wanawake na kuwaweka gerezani.
5Kuhani mkuu na baraza lote la wazee wa Wayahudi wanaweza kuwathibitishia hili. Wakati mmoja viongozi hawa walinipa barua. Barua hizo waliandikiwa ndugu zetu Wayahudi katika mji wa Dameski. Nilikuwa naenda huko kuwakamata wafuasi wa Yesu na kuwaleta Yerusalemu ili waadhibiwe.
6Lakini kitu fulani kilinitokea nikiwa njiani kwenda Dameski. Ilipokuwa inakaribia mchana na nilikuwa karibu na mji wa Dameski. Ghafla mwanga kutoka mbinguni ulining'aria kunizunguka.
7Nilianguka chini na nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli kwa nini unanitesa?’
8Niliuliza, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ Sauti ikasema, ‘Mimi ni Yesu kutoka Nazareti, unayemtesa.’
9Watu waliokuwa pamoja nami hawakuisikia sauti lakini waliona mwanga.
10Nilisema, ‘Nifanye nini Bwana?’ Bwana alinijibu, ‘Simama na uingie Dameski. Humo utawaambia yote niliyopanga uyafanye.’
11Sikuweza kuona kwa sababu mwanga ule angavu ulinilemaza macho. Hivyo wale watu waliokuwa pamoja nami waliniongoza kuingia mjini Dameski.
12Alikuwepo mtu mmoja katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania. Mtu huyu alikuwa mcha Mungu na aliitii Sheria ya Musa na Wayahudi wote walioishi kule walimheshimu.[#22:12 Katika Matendo ya Mitume wapo watu watatu waliotumia jina hili. Tazama Mdo 5:1; 23:2 kwa ajili ya wale wengine wawili.]
13Alikuja kwangu na kuniambia, ‘Sauli, ndugu yangu, tazama juu na uone tena!’ Ghafla niliweza kumwona.
14Anania aliniambia, ‘Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu alikuchagua wewe tangu zamani kuujua mpango wake. Amekuchagua wewe kumwona Mwenye Haki wake na kusikia maneno kutoka kwake.
15Utakuwa shahidi wake kwa watu wote. Utawaambia ulichoona na kusikia.
16Sasa usisubiri zaidi. Simama, ubatizwe na usafishwe dhambi zako, mwamini Yesu ili akuokoe.’[#22:16 Kwa maana ya kawaida, “kuliitia jina lake”, kuonesha imani katika Yesu kwa kumwabudu au kumwomba kwa ajili ya msaada.]
17Baadaye, nilirudi Yerusalemu. Nilipokuwa naomba katika eneo la hekalu, nikaona maono.
18Nilimwona Yesu, naye akaniambia, ‘Haraka, ondoka Yerusalemu sasa hivi! Watu hapa hawataukubali ukweli unaowaambia kuhusu mimi.’
19Nilisema, ‘Lakini, Bwana, Wayahudi wanajua kuwa mimi ndiye niliyewafunga gerezani na kuwapiga wale wanaokuamini wewe. Nilikwenda kwenye masinagogi yote kuwatafuta na kuwakamata Wayahudi wanaokuamini wewe.
20Watu wanajua pia kuwa nilikuwepo wakati Stefano shahidi wako, alipouawa. Nilisimama pale na kukubaliana nao kuwa wamwue. Nilishikilia hata mavazi ya watu waliokuwa wanamwua!’
21Lakini Yesu akaniambia, ‘Ondoka sasa. Nitakutuma mbali sana kwa watu wasio Wayahudi.’”
22Watu waliacha kusikiliza Paulo aliposema jambo hili la mwisho. Walipasa sauti wote, wakisema, “Mwondosheni mtu huyu! Hastahili kuishi katika dunia hii tena.”
23Waliendelea kupiga kelele, wakichana nguo zao na kurusha mavumbi juu.[#22:23 Matendo haya yalikuwa ishara ya hasira kali sana.]
24Ndipo kamanda akawaambia askari wamwingize Paulo kwenye jengo la jeshi na wampige. Alitaka kumlazimisha Paulo aeleze ni kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna ile.
25Askari walipokuwa wanamfunga Paulo, wakijiandaa kumpiga alimwuliza ofisa wa jeshi, “Je! mna haki ya kumpiga raia wa Rumi ambaye hajathibitika kuwa na hatia?”[#22:25 Sheria Rumi ilisema kwamba raia wa Rumi hawezi kuadhibiwa kabla ya kushitakiwa na kuhukumiwa baada ya kukutwa na hatia. Tazama pia Mdo 23:27.]
26Ofisa aliposikia hili, alikwenda kwa kamanda na kumwambia. Ofisa alisema, “Unafahamu unalolifanya? Mtu huyu ni raia wa Rumi!”
27Kamanda akaenda kwa Paulo na kusema, “Niambie kwa hakika, ‘Je! wewe ni raia wa Rumi?’”
Paulo akajibu, “Ndiyo.”
28Kamanda akasema, “Nililipa pesa nyingi kuwa raia wa Rumi.”
Lakini Paulo akasema, “Nilizaliwa raia wa Rumi.”
29Ghafla watu waliokuwa wanajiandaa kumwuliza maswali Paulo waliondoka. Kamanda aliogopa kwa sababu alikuwa ameshamfunga Paulo kwa minyororo na ni raia wa Rumi.
30Siku iliyofuata kamanda alitaka kujua ni kwa nini Wayahudi wanamshitaki Paulo. Hivyo aliamuru viongozi wa makuhani na baraza kuu lote kukutana pamoja. Alimfungua Paulo minyororo na kumleta mbele ya baraza.