The chat will start when you send the first message.
1Tulipokuwa salama nchi kavu, tukatambua kuwa kisiwa kile kinaitwa Malta.
2Watu walioishi pale walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa baridi sana, hivyo walitengeneza moto na kutukaribisha sote.
3Paulo alikusanya kuni nyingi kwa ajili ya moto. Alipokuwa akiweka kuni kwenye moto, nyoka mwenye sumu kali akajitokeza kwa sababu ya joto na kumuuma kwenye mkono.
4Wenyeji wa kisiwa kile walipomwona nyoka ananing'inia kwenye mkono wa Paulo, walisema, “Mtu huyu lazima ni mwuaji! Hakufa baharini, lakini Haki hataki aishi.”[#28:4 Wenyeji wa kisiwa kile waliamini kuwa kuna mungu mke aliyeitwa Haki ambaye angewaadhibu waovu.]
5Lakini Paulo alimku'ngutia nyoka kwenye moto na hakudhurika.
6Watu wakadhani atavimba au ataanguka na kufa. Walisubiri na kumwangalia kwa muda mrefu, lakini hakuna kibaya kilichomtokea. Hivyo wakabadili mawazo yao. Wakasema, “Paulo ni mungu!”
7Yalikuwepo mashamba kuzunguka eneo lile. Yaliyomilikiwa na ofisa wa juu sana wa Rumi katika kisiwa hicho aliyeitwa Pablio. Alitukaribisha nyumbani kwake na alikuwa mwema sana kwetu. Tulikaa nyumbani kwake kwa siku tatu.
8Baba yake Pablio alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa na homa na alikuwa anaharisha damu, lakini Paulo alikwenda kwake na kumuombea. Aliweka mikono juu yake naye akapona.
9Baada ya hili kutokea, wagonjwa wengine wote kisiwani walikuja kwa Paulo, naye aliwaombea na wakaponywa pia.
10-11Watu katika kisiwa hiki walituheshimu sana. Na baada ya kuwa pale kwa miezi mitatu, tukawa tayari kuondoka, walitupa kila kitu tulichohitaji kwa ajili ya safari yetu.
Tulipanda meli iliyotoka Iskanderia iliyokaa katika kisiwa cha Malta wakati majira ya baridi. Mbele ya meli kulikuwa alama ya miungu pacha.
12Tulisimama katika mji wa Sirakuse. Tulikaa pale kwa siku tatu kisha tukaondoka.
13Tulifika katika mji wa Regio. Siku iliyofuata upepo ulianza kuvuma kutokea kusini-magharibi, hivyo tuliweza kuondoka. Baada ya siku moja tukafika katika mji wa Puteoli.
14Tuliwapata baadhi ya waamini pale, walituomba tukae nao kwa wiki moja. Mwishowe tulifika Rumi.
15Ndugu na dada waliokaa Rumi walisikia habari zetu, walikuja kutupokea kwenye Soko la Apio na kwenye Migahawa Mitatu. Paulo alipowaona waamini hawa, alimshukuru Mungu na alifarijika.[#28:15 Mji ulio kama maili 43 (kilomita 69) kutoka mji wa Rumi.; #28:15 Mji ulio kama maili 30 (kilomita 48) kutoka mji wa Rumi.]
16Tulipofika Rumi, Paulo aliruhisiwa kuishi peke yake. Lakini askari alikaa pamoja naye kumlinda.
17Siku tatu baadaye Paulo aliagiza baadhi ya Wayahudi muhimu waje kwake. Walipokusanyika, akasema, “Ndugu zangu, sijafanya lolote kinyume na watu wetu au kinyume na desturi za baba zetu. Lakini nilikamatwa Yerusalemu na kukabidhiwa kwa Warumi.
18Waliniuliza maswali mengi, lakini hawakupata sababu yoyote kwa nini niuawe. Hivyo walitaka kuniachia huru.
19Lakini Wayahudi kule hawakutaka hilo. Hivyo ilinibidi niombe kuja Rumi kuweka mashitaka yangu mbele ya Kaisari. Kwa kufanya hivi haimaanishi kuwa ninawashutumu watu wangu kwa kufanya chochote kibaya.
20Ndiyo sababu nilitaka kuonana na kuzungumza nanyi. Nimefungwa kwa minyororo hii kwa sababu ninaamini katika tumaini la Israeli.”
21Wayahudi walimjibu Paulo, “Hakuna barua tuliyoipokea kutoka Uyahudi kuhusu wewe. Hakuna ndugu yetu yeyote Myahudi aliyesafiri kutoka huko aliyeleta habari zako au kutwambia chochote kibaya juu yako.
22Tunataka kusikia mawazo yako. Tunafahamu kuwa watu kila mahali wanapinga kundi hili jipya.”
23Paulo na Wayahudi walichagua siku kwa ajili ya mkutano. Siku hiyo Wayahudi wengi walikutana na Paulo katika nyumba yake. Aliwaambia kwa siku nzima, akawafafanulia kuhusu ufalme wa Mungu. Alitumia Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kuwashawishi kumwamini Yesu.
24Baadhi ya Wayahudi waliamini alichosema, lakini wengine hawakuamini.
25Walibishana wao wenyewe na wakaanza kuondoka. Lakini aliwaambia kitu kimoja zaidi: “Roho Mtakatifu aliwaambia ukweli baba zenu kupitia nabii Isaya, aliposema,
26‘Nenda kwa watu hawa na uwaambie:
Mtasikiliza na kusikiliza,
lakini hamtaelewa.
Mtatazama na kutazama,
lakini hakika hamtaona.
27Watu hawa hawawezi kuelewa.
Masikio yao yamezibwa.
Na macho yao yamefumbwa.
Hivyo hawawezi kuona kwa macho yao,
au kusikia kwa masikio yao;
au kuelewa kwa akili zao;
au kuelewa kwa akili zao.
Ikiwa wangeelewa, wangeweza kunirudia,
na ningewaponya.’
28Ninataka ninyi Wayahudi mjue kuwa Mungu ameupeleka wokovu wake kwa watu wasio Wayahudi. Watasikia!”
30Paulo alikaa katika nyumba yake mwenyewe aliyopanga kwa miaka miwili kamili. Aliwakaribisha watu wote waliokuja kumtembelea.
31Aliwaambia kuhusu ufalme wa Mungu na kuwafundisha kuhusu Bwana Yesu Kristo. Alikuwa na ujasiri sana, na hakuna aliyejaribu kumzuia asizungumze.