Wagalatia 3

Wagalatia 3

Baraka za Mungu Huja Kwa Imani

1Ninyi watu wa Galatia, je mmepoteza fahamu zenu? Nilidhani mmeelewa kwa nini Yesu Kristo alisulubiwa msalabani! Niliwaeleza wazi kabisa jambo hilo, kama vile kuchora na kupaka rangi picha mbele ya macho yenu. Je! kuna mtu yeyote aliyewaloga mkasahau?

2Niambieni jambo hili moja: Ni jinsi gani mlimpokea Roho? Je! mlimpokea Roho kwa kufuata sheria? Hapana, mlimpokea Roho kwa sababu ya ujumbe kuhusu Yesu unaoleta imani.

3Mliyaanza maisha yenu mapya pamoja na Roho. Inakuwaje sasa mdhani kuwa mnaweza kukamilishwa na kitu kinyonge kama tohara kilichofanyika katika miili yenu? Basi mmepoteza fahamu zenu![#3:3 Kwa maana ya kawaida, “katika mwili”. Paulo kila mara ametumia msemo huu akimaanisha udhaifu wa kutenda dhambi wa mwanadamu. Lakini katika barua hii, anatumia msemo huu hasa kwa maana ya tohara (6:12,13), jambo ambalo lilikuwa katika kitovu cha hoja za Paulo dhidi ya wale waliokuwa “wakiwayumbisha” waamini wa Galatia (tazama 1:7).]

4Je! mlipata uzoefu huo mwingi pasipo manufaa yoyote? Sidhani kama hivyo ndivyo!

5Je! Mungu anawapa ninyi Roho na kutenda miujiza miongoni mwenu kwa kuwa mnaifuata sheria? Hapana sivyo! Mungu anawapa ninyi baraka hizi kwa njia ya ujumbe unaoleta imani katika kumwamini Yesu.

6Maandiko yanasema kitu hicho hicho kuhusu Abrahamu. “Abrahamu alimwamini Mungu, na Mungu akaikubali imani yake na akamhesabia haki.”[#Mwa 15:6]

7Hivyo mnapaswa kuelewa kuwa watoto sahihi wa Abrahamu ni wale walio na imani.

8Maandiko yalieleza ambacho kingetokea katika siku zinazokuja. Maandiko haya yalisema kwamba Mungu angewafanya wasio Wayahudi kuwa wenye haki kwa njia ya imani. Mungu alizisema Habari Njema hizi kwa Abrahamu kabla haijatokea. Mungu alimwambia Abrahamu, “Kwa kukubariki wewe, nitawabariki watu wote duniani.”[#Mwa 12:3; 18:18]

9Kwa hiyo, wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu ndiyo wanaobarikiwa pamoja na Abrahamu aliyekuwa mwaminifu.

10Lakini watu wale wanaodhani kuwa kutii sheria ndicho kitu muhimu sana daima hukaa chini ya tishio la laana. Kama vile Maandiko yanavyosema, “Amelaaniwa mtu yeyote atakayeacha kuzishika na kuzitii sheria hizi zote.”[#Kum 27:26]

11Hivyo ni dhahiri kuwa hakuna anayeweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Maandiko yanasema, “Mwenye haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.”[#Hab 2:4]

12Sheria haitegemei imani. Hapana, inasema kuwa njia pekee ambayo mtu anaweza kupata uzima kwa njia ya sheria ni kwa kutii amri zake.[#3:12 Tazama Law 18:5.]

13Sheria inasema kuwa sisi Wayahudi tuko chini ya laana kwa kutokuitii daima. Lakini Kristo alituweka huru kutoka katika laana hiyo. Alikubali kulaaniwa na sheria ili atuokoe. Maandiko yanasema, “Yeyote anayening'inizwa mtini yuko chini ya laana.”[#3:13 Tazama Kum 21:22-23.; #Kum 21:23]

14Kwa sababu ya yale aliyoyafanya Kristo Yesu, baraka ambazo Mungu alimwahidi Abrahamu zilitolewa pia kwa wasio Wayahudi. Kristo alikufa ili kwamba kwa kumwamini sisi sote, Wayahudi na wasio Wayahudi, tuweze kumpokea Roho ambaye Mungu aliahidi.

Sheria na Ahadi

15Ndugu zangu, hebu niwape mfano kutoka maisha ya kila siku: Fikiri kuhusu maagano ambayo mtu hukubaliana na mwingine. Baada ya maagano hayo kufanywa rasmi, hakuna anayeweza kuongeza chochote kwenye maagano hayo na hakuna anayeweza kulipuuza.

16Mungu aliweka agano kwa Abrahamu na uzao wake. Maandiko hayasemi, “na kwa ajili ya uzao wenu”. Hilo lingekuwa na maana ya watu wengi. Lakini linasema, “na kwa uzao wako”. Hiyo ina maana ya uzao mmoja tu, na uzao huo ni Kristo.

17Hii ndiyo maana yangu: Agano ambalo Mungu aliliweka na Abrahamu lilifanywa rasmi na Mungu muda mrefu kabla ya kuja kwa sheria. Sheria ilikuja miaka 430 baadaye. Hivyo sheria haingeweza kulifuta agano hilo na kuibadili ahadi ya Mungu.

18Baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake hazipatikani kwa njia ya sheria. Ikiwa ingekuwa hivyo, basi isingekuwa ahadi ya Mungu inayotuletea sisi baraka hiyo. Lakini Mungu aliitoa bure baraka yake kwa Ibrahamu kama agano.

19Hivyo kwa nini sheria ilitolewa? Sheria ililetwa baadaye kwa sababu ya makosa wanayotenda watu. Lakini sheria ingeendelea kutumika hadi kuja kwa Uzao wa Abrahamu. Huyu ni Uzao unaotajwa katika agano lililotolewa na Mungu. Lakini sheria ilitolewa kupitia malaika na malaika walimtumia Musa kama mpatanishi wa kuwapa watu sheria.[#3:19 Sheria ilitambua kosa (tazama mstari wa 22) na pia ilizuia kosa lisitendeke (tazama mstari wa 23-24).]

20Hivyo mpatanishi anahitajika pale ambapo upande mmoja unapaswa kufikia maagano. Lakini Mungu ambaye ni mmoja, hakumtumia mpatanishi alipompa ahadi Abrahamu.[#3:20 Kwa maana ya kawaida, “Lakini mpatanishi si kwa ajili ya mmoja, lakini Mungu ni mmoja.”]

Lengo la Sheria ya Musa

21Je! hili lamaanisha kwamba sheria hutenda kazi kinyume na ahadi za Mungu? La hasha. Sheria iliyotolewa kamwe haikuwa na uwezo wa kuwaletea watu maisha mapya. Ingekuwa hivyo, basi tungehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria.

22Lakini hilo halikuwa kusudi la sheria. Maandiko yanauweka ulimwengu wote chini ya udhibiti wa dhambi kama aina ya kifungo gerezani. Ili kile ambacho Mungu aliahidi kipokelewe kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hii hutolewa kwa wale wanaomwamini.[#3:22 Au “uaminifu wake”.]

23Kabla ya aliye mwaminifu kuja, sheria ilituweka sisi kama wafungwa. Hatukuwa huru hadi imani hii inayokuja ilipofunuliwa kwetu.[#3:23 Au “imani ya Yesu”.]

24Nina maana kuwa sheria ilikuwa ni mlezi aliyetusimamia tu hadi Kristo alipokuja. Baada ya kuja kwake, tungefanyika kuwa wenye haki mbele za Mungu kwa njia ya imani.[#3:24 Ina maana kama ile ya mlezi wa watoto yaani yaya; Kwa Kiyunani namaanisha mtu, kwa kawaida aliyekuwa mtumwa, aliyemsindikiza mvulana mdogo kwenda shule toka nyumbani na kuhakikisha ya kwamba mvulana yule anaenenda vizuri na hapati matatizo.]

25Sasa kwa sababu imani hii imekuja, hatuhitaji tena kusimamiwa na kulelewa na sheria.

26Hii ni kwa sababu ninyi nyote ni mali ya Kristo Yesu na ni watoto wa Mungu kwa njia ya imani.

27Ndiyo, nyote mlibatizwa ili muunganike na Kristo. Hivyo sasa Kristo anawafunika kabisa kama kubadilisha nguo mpya kabisa.

28Sasa, ndani ya Kristo haijalishi kama wewe u Myahudi au Myunani, mtumwa au huru, mwanaume au mwanamke. Wote mko sawa katika Kristo Yesu.

29Na kwa vile ninyi ni wa Kristo, hivyo ninyi wazaliwa wa Ibrahamu. Ninyi ndiyo mtakaopokea baraka zote ambazo Mungu alimwahidi Abrahamu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International