Wagalatia 6

Wagalatia 6

Tuishi kwa Kusaidiana Sisi kwa Sisi

1Ndugu zangu, ikiwa mmoja wenu atakosea, ninyi mnaomfuata Roho mnapaswa kumwendea yule anayetenda dhambi. Msaidieni mtu huyo awe mwenye haki tena. Mfanye hivyo kwa njia ya upole, na muwe waangalifu, kwa maana nanyi pia mnaweza kujaribiwa kutenda dhambi.

2Msaidiane ninyi kwa ninyi katika kubeba mizigo yenu. Mnapofanya hivi, mtakuwa mnatimiza yote ambayo sheria ya Kristo imewaagiza kufanya.

3Maana mtu akijiona kuwa yeye ni wa muhimu sana na kumbe sio wa muhimu, anajidanganya mwenyewe.

4Kila mmoja aipime kazi yake mwenyewe kuona ikiwa kuna chochote cha kujivunia. Kama ndivyo, uyatunze hayo moyoni mwako wala usijilinganishe na mtu mwingine yeyote.

5Maana sisi sote tunawajibika kwa yale tunayofanya.

Msiache Kutenda Mema

6Yule anayefundishwa neno la Mungu anapaswa kumshirikisha mwalimu wake mambo mema aliyonayo.

7Ikiwa mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu, mtakuwa mnajidanganya wenyewe. Mtavuna yale mnayopanda.

8Yule anayepanda kwa kuiridhisha nafsi yake ya dhambi, mavuno yatakayopatikana ni uharibifu kabisa. Lakini mkipanda kwa kuiridhisha Roho, mavuno yenu katika Roho yatakuwa uzima wa milele.

9Hatupaswi kuchoka katika kutenda mema. Tutapata mavuno yetu kwa wakati sahihi, tusipokata tamaa.

10Tunapokuwa na nafasi ya kumtendea mema kila mtu, tufanye hivyo. Lakini tuzingatie zaidi kuwatendea mema wale walio wa familia ya waamini.

Paulo Amalizia Barua Yake

11Huu ni mwandiko wa mkono wangu mwenyewe. Mnaweza kuona jinsi herufi zilivyo kubwa.[#6:11 Sasa Paulo amechukua kalamu kutoka kwa mwandishi/katibu wake ili mwenyewe aandike sehemu ya mwisho ya barua. Herufi kubwa labda inawezekana ni kwa ajili ya kusisitiza muhtasari unaofuata wa hoja zake kuu, kama vile unapotumia wino mzito au kwa herufi kubwa leo.]

12Watu wale wanaojaribu kuwalazimisha ninyi kutahiriwa wanafanya hivyo ili wawaridhishe Wayahudi wenzao. Wanaogopa wasije wakateswa kwa sababu ya msalaba wa Kristo.[#6:12 Paulo anatumia msalaba kama kielelezo cha Habari Njema, habari ya kifo cha Kristo kwa ajili ya kuwaweka watu huru mbali na dhambi. Msalaba (Kifo cha Kristo) kilikuwa njia ya Mungu ya kuwaokoa watu. Pia katika mstari wa 14.]

13Maana hata wale waliotahiriwa hawaitii sheria. Na bado wanawataka ninyi mtahiriwe ili waweze kujisifu kwa ajili ya yale waliyowatendea ninyi.

14Mimi nisijisifu kwa ajili ya mambo kama haya. Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo sababu pekee ya kujivuna kwangu. Kupitia kifo cha Yesu msalabani ulimwengu ukafa kwangu, nami nimeufia ulimwengu.[#6:14 Kwa maana ya kawaida, “umesulubishwa”.]

15Haijalishi kwamba mtu ametahiriwa au hajatahiriwa. Kinachojalisha ni uumbaji mpya wa Mungu katika Kristo.[#6:15 Kwa maana ya kawaida, “kiumbe kipya”. Tazama 2 Kor 5:17.]

16Amani iwe kwa wale wote wanaoifuata njia hii mpya. Na rehema za Mungu ziwe juu ya watu wake Israeli.

17Kwa hiyo msinitaabishe kwa namna yoyote. Nina makovu mwilini mwangu yanayoonyesha kuwa mimi ni wa Yesu.[#6:17 Mara nyingi Paulo alikuwa anapigwa na watu waliokuwa wanajaribu kumzuia kufundisha kuhusu Kristo. Makovu yalitokana na mapigo hayo.]

18Ndugu na dada zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International