Ufunuo 11

Ufunuo 11

Mashahidi Wawili

1Kisha nilipewa fimbo ya kupimia, ndefu kama fimbo ya kutembelea. Nikaambiwa, “Nenda ukalipime hekalu la Mungu na madhabahu na uwahesabu watu wanaoabudu humo.[#11:1 Nyumba ya Mungu. Mahali ambapo watu wa Mungu humwabudu na kumtumikia. Yohana hapa analitazama kama jengo maalumu katika mji wa Yerusalemu kwa ajili ya ibada za Kiyahudi. Pia katika mstari wa 19.]

2Lakini usipime eneo lililo nje ya hekalu. Liache. Eneo hilo wamepewa watu wasio wa Mungu. Wataonesha nguvu zao juu ya mji mtakatifu kwa miezi 42.

3Nami nitawapa nguvu mashahidi wangu wawili, watatabiri kwa siku 1,260. Nao watakuwa wamevaa magunia.”

4Mashahidi hawa wawili ni mizeituni miwili na vinara viwili vya taa vinavyosimama mbele za Bwana wa dunia.

5Ikiwa mtu yeyote atajaribu kuwadhuru mashahidi hawa, moto utatoka katika vinywa vyao na kuwaua adui zao. Yeyote atakaye jaribu kuwadhuru atakufa.

6Mashahidi hawa wana nguvu ya kuzuia mvua isinyeshe katika wakati ambao watakuwa wanatabiri. Pia wana uwezo wa kugeuza maji kuwa damu. Wana uwezo wa kutuma kila aina ya pigo duniani. Wanaweza kufanya hivi kadri wanavyotaka.

7Mashahidi wawili watakapomaliza kuutangaza ujumbe wao, mnyama atokaye kuzimu atapigana nao. Atawashinda na kuwaua.

8Miili ya mashahidi hawa wawili italala kwenye mtaa wa mji mkuu. Mji huu unaitwa Sodoma na Misri. Majina ya mji huu yana maana maalumu. Huu ni mji ambako Bwana aliuawa.

9Watu kutoka kila asili, kabila, lugha na taifa wataiangalia miili ya mashahidi hawa wawili kwa siku tatu na nusu. Watu watakataa kuwazika.

10Na Kila aishiye duniani atafurahi kwa sababu mashahidi hawa wawili wamekufa. Watu watafanya sherehe na kupeana zawadi kwa sababu manabii hawa wawili walileta mateso mengi kwa watu waishio duniani.

11Lakini baada ya siku tatu na nusu, Mungu akawarudishia uhai mashahidi hawa wawili. Wakasimama kwa miguu yao. Na wale waliowaona wakajaa hofu.

12Kisha mashahidi wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikisema, “Njooni huku juu!” Na wote wawili wakaenda juu mbinguni katika wingu, adui zao wakiangalia wanavyokwenda.

13Katika wakati huo huo kulitokea tetemeko kuu la ardhi. Sehemu ya kumi ya mji ikateketea, na watu elfu saba wakafa. Wale ambao hawakufa waliogopa sana. Wakampa utukufu Mungu wa mbinguni.

14Kitisho cha pili kimepita. Kitisho cha tatu kinakuja haraka.

Mlio wa tarumbeta ya Saba

15Malaika wa saba alipopuliza tarumbeta yake, zikatokea sauti kuu mbinguni, zikasema:

“Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Masihi wake sasa.

Na atatawala milele na milele.”

16Kisha wazee 24 wakaanguka chini nyuso zao zikiwa chini wakamwabudu Mungu. Hawa ni wazee ambao wanakaa kwenye viti vyao vya heshima mbele za Mungu.

17Wazee wakasema:

“Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi.

Wewe ndiye uliyepo na ambaye daima umekuwepo.

Tunakushukuru kwa sababu umetumia uweza wako mkuu

na umeanza kutawala.

18Mataifa walikasirika,

lakini sasa ni wakati kwa ajili ya hasira yako.

Sasa ni wakati wa waliokufa kuhukumiwa.

Ni wakati wa kuwapa thawabu watumishi wako, manabii,

na kuwapa thawabu watu wako watakatifu,

wakubwa na wadogo, wanaokuheshimu wewe.

Ni wakati wa kuwaangamiza watu wanaoiangamiza dunia!”

19Kisha hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa. Sanduku la Agano likaonekana ndani ya hekalu lake. Kisha kukatokea miali ya radi na miungurumo ya radi, kelele, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International