The chat will start when you send the first message.
1Hivyo, je, mnadhani inatupasa tuendelee kutenda dhambi ili Mungu atupe neema nyingi zaidi na zaidi?
2Hapana! Utu wetu wa zamani wa dhambi ulikwisha. Umekufa. Je! tutaendeleaje kuishi katika dhambi?
3Je! mmesahau kwamba sisi sote tulifanyika sehemu ya Kristo Yesu tulipobatizwa? Katika ubatizo wetu tulishiriki katika kifo chake.
4Hivyo, tulipobatizwa, tulizikwa pamoja na Kristo na kushiriki katika kifo chake. Na kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa nguvu ya ajabu ya Baba, ndivyo nasi tunaweza kuishi maisha mapya sasa.
5Kristo alikufa, nasi tumeunganishwa pamoja naye kwa kufa kama yeye alivyokufa. Kwa hiyo tutaunganishwa pamoja naye kwa kufufuka kutoka katika kifo kama yeye alivyofanya.
6Tunajua kuwa utu wetu wa zamani ulikufa msalabani pamoja naye. Hivyo ndivyo maisha ya utumwa tuliyokuwa nayo yalivyoangamizwa ili tusiendelee kuitumikia dhambi tena.
7Yeyote aliyekufa amewekwa huru kutoka katika nguvu za dhambi.
8Ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunajua kwamba tutaishi pamoja naye pia.
9Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na tunajua kuwa hawezi kufa tena. Sasa mauti haina nguvu juu yake.
10Ndiyo, Kristo alipokufa, alikufa ili aishinde nguvu ya dhambi mara moja, na siyo mara nyingine tena. Sasa anao uzima mpya, na uzima wake huo upo kwa nguvu za Mungu.
11Kwa namna hiyo hiyo, mnapaswa kujiona kama mliokufa kwa dhambi na mlio hai kwa nguvu za Mungu kupitia Kristo Yesu.
12Mwili mlionao katika uhai wenu wa sasa hapa duniani utakufa. Msiruhusu dhambi iutawale na kuwafanya ninyi kuzitumikia tamaa zake.
13Msiitoe sehemu ya miili yenu kwa dhambi kwa ajili ya kutumika kutenda maovu. Jitoeni kwa Mungu, kama watu waliokufa lakini walio hai. Toeni sehemu za miili yenu kwa Mungu ili zitumiwe kwa kutenda mema.
14Dhambi haitakuwa mtawala wenu, kwa sababu hamko chini ya sheria. Sasa mnaishi chini ya neema ya Mungu.
15Hivyo tufanye nini? Je! tutende dhambi kwa sababu tuko chini ya neema na siyo chini ya sheria? Hapana!
16Hakika mnajua kuwa unakuwa mtumwa wa jambo lolote unaojitoa kulifanya. Chochote au yeyote unayemtii atakuwa bwana wako. Unaweza kufuata dhambi, au kumtii Mungu. Kufuata dhambi kunaleta kifo cha kiroho, lakini kumtii Mungu kunakufanya uhesabiwe na Mungu.
17Hapo zamani mlikuwa watumwa wa dhambi na dhambi iliwatawala. Lakini ashukuriwe Mungu, mlitii kwa hiyari mafundisho yote aliyowaelekeza.
18Mliwekwa huru kutoka katika dhambi, na sasa ninyi ni watumwa wa uaminifu wa wema wa Mungu.
19Natumia dhana hii ya utumwa kutoka katika maisha ya kila siku kwa sababu mnahitaji msaada katika kuielewa kweli hii ya kiroho. Zamani mliitoa sehemu ya miili yenu kuwa watumwa wa mawazo yenu yaliyo machafu na maovu. Matokeo yake mliishi kwa ajili ya dhambi tu. Kwa njia hiyo hiyo, sasa mnapaswa kujitoa wenyewe kama watumwa wa uaminifu wa wema wa Mungu ili mweze kufaa kabisa kwa utumishi kwake.
20Zamani mlikuwa watumwa wa dhambi, na wala hamkufikiri juu ya kutenda haki.
21Mlifanya mambo maovu, na sasa mnaaibishwa kwa yale mliyotenda. Je! mambo haya yaliwasaidia? Hapana, yalileta kifo tu.
22Lakini sasa mko huru dhidi ya dhambi. Mmekuwa watumwa wa Mungu, na mnaishi kwa ajili ya Mungu tu. Hili litawaletea uzima wa milele.
23Watu wanapotenda dhambi, wanapokea malipo ya dhambi, ambayo ni kifo. Lakini Mungu huwapa watu wake zawadi ya bure, yaani uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.