The chat will start when you send the first message.
1Uwakumbushe watu wako ya kuwa wanapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya watawala wao na uongozi wa dola. Wanapaswa kuwatii viongozi hao na kuwa tayari kufanya kila jema wanaloweza.
2Waambie hawapaswi kumtukana mtu yeyote, bali wawe wema na wapole kwa watu wote.
3Hapo zamani hata sisi tulikuwa wajinga, wakaidi na tulidanganyika. Tulikuwa watumwa kwa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu. Tulichukiwa na watu nasi tukachukiana wenyewe kwa wenyewe.
4Lakini Mungu Mwokozi wetu alitudhihirishia
wema na upendo alionao kwa wanadamu.
5Alituokoa kwa sababu yeye ni mwenye rehema,
siyo kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda na kupata kibali chake,
bali ni kwa rehema yake.
Yeye aliziosha dhambi zetu,
akatupa maisha mapya kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Ikawa kama kuzaliwa kwa mara ya pili.
6Mungu ametumiminia Roho Mtakatifu kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu.
7Kwa neema yake Mungu alituweka huru mbali na dhambi.
Akatufanya kuwa warithi wake tulio na tumaini la uzima wa milele.
8Huu ni usemi wa kuaminiwa. Nawataka ninyi kuyasisitiza mambo haya, ili wale waliokwisha kumwamini Mungu waweze kujitoa katika matendo mema. Mambo haya ni mazuri na ya kuwanufaisha watu.
9Lakini yaepuke mabishano ya kipumbavu, majadiliano kuhusu koo, mabishano na ugomvi kuhusu Sheria, maana hayana faida na hayafai.
10Mwepuke mtu anayesababisha matengano baada ya onyo la kwanza na la pili,
11kwa sababu unajua kuwa mtu wa jinsi hiyo amepotoka na anatenda dhambi. Amejihukumu mwenyewe.
12Nilipomtuma kwako Artema au Tikiko, jitahidi kuja Nikopoli ili kuonana nami, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa msimu wa baridi.
13Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena pamoja na Apolo kwa lo lote watakalohitaji kwa ajili ya safari yao, ili wasipungukiwe na kitu cho chote.
14Watu wetu wanapaswa kujifunza kujihusisha katika kutenda mema ili kusaidia kukitokea mahitaji, ili wasiwe watu wasiokuwa na manufaa.
15Wote nilio pamoja nami wanakusalimu. Uwasalimu wote wanaotupenda katika imani.
Neema ya Mungu iwe nanyi nyote.